Jumatatu , 28th Mar , 2016

Zaidi ya silaha 96, zimesalimishwa katika tarafa ya Loliondo, Wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa huo Felix Ntibenda kuwataka wananchi kusalimisha silaha zao.

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda.

Akizungumzia hatua hiyo Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mngandilwa, amesema katika silaha hizo 96 zilizosalimishwa na wananchi Silaha 6 ni za kivita ambazo zilikua zinamilikiwa na wananchi kinyume cha sheria.

Mratibu wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na upingaji wa umilikaji silaha kiholela nchini, Dkt. Peter Mkomala amesema wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja na serikali katika kukomesha tatizo hilo.

Dkt. Mkomala amesema kuwa katika tafiti alizofanya katika mikoa ya Kigoma na Kagera amegundua kuna watu wengi sana wanamiliki silaha kinyume cha sheria hivyo serikali inapaswa kuzikagua upya silaha hizo na kuangalia mihuri ya silaha hizo kama ni sahihi au la.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Felix Ntibenda amesema kuwa Mkoa wa Arusha unafahamika kuwa na silaha nyingi jambo ambalo aliamuru kuanzia mwezi wa pili kufanya uhakiki wa silaha hasa maeneo ya Loliondo ambapo hutokea mapigano ya kulipizana kisasi.