Alhamisi , 21st Sep , 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kujiingizia kipato cha kuweza kumudu gharama za maisha.

Amesema ni wajibu wa kila mmoja kwa nafasi yake kufanya kazi kwa bidii ili aweze kupata fedha za kumuwezesha kumudu huduma muhimu katika jamii.

Mhe. Simbachawene ametoa wito huo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mbuga iliyopo katika  Jimbo la Kibakwe, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo lake.

"Ukiwa huna fedha ikitokea umeumwa, utashindwa kupata matibabu na kuweza kuhatarisha uhai wako, hivyo ni bora kila mmoja wetu akahakikisha anafanya kazi ili apate fedha za kumudu mahitaji muhimu," amesema Waziri Simbachawene.

Amesema kila mwananchi kwa nafasi yake ni muhimu akahakikisha anajikita katika kuzalisha mali ili aweze kupata fedha.

Amefafanua kuwa hakuna maisha magumu kama inavyodaiwa na watu wengi isipokuwa mahitaji ya  fedha yameongezeka kutokana na kukua kwa maendeleo.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene amewataka wananchi hao kuacha tabia ya  kukaa bila kufanya kazi badala yake waitumie ardhi yenye rutuba waliyojaaliwa kuwa nayo kwa  ajili ya shughuli za kilimo ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Amesema maendeleo ni mchakato ambapo kila huduma inayoletwa inahitaji fedha, akitolea mfano ili uingize umeme katika nyumba yako unahitaji uwe na fedha.

Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene ameutaka uongozi wa vijiji vinavyounda Kata ya  Mbuga  kuunda sheria ndogo ndogo za kupiga marufuku unywaji pombe nyakati za asubuhi ili muda huo utumike katika kuzalisha mali.

Amesema ni aibu kuona vijana hawafanyi kazi wanachowaza ni kunywa pombe kuanzia asubuhi hadi jioni.

Ameeleza kuwa ni vyema sehemu hizo za kuuzia pombe zisiwe za vificho huku akitaka   uuzwaji huo wa pombe uanze kufanyika jioni wakati wananchi walio wengi wakiwa tayari wameshafanya kazi.