Alhamisi , 23rd Mei , 2019

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amepokea taarifa ya Kamati ya Maadili ya Bunge ambayo iliketi kwa ajili ya kumhoji Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika PAP.

Mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele.

Taarifa ya hukumu ya Mbunge huyo imewasilishwa bungeni leo na Almas Maige ambaye amewasilisha ripoti hiyo leo wakati wa kikao cha Bunge jijini Dodoma.

"Kwa niaba ya Mwenyekiti Kamati ya Maadili ya Bunge, naomba kuwasilisha mezani taarifa  kuhusu Julius Masele ya kulidharau Bunge, mamlaka ya spika, kulifedhesha Bunge na kuchonganisha mihimili ya dola", amesema Maige.

Mei 16, 2019, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliibua madai kuhusiana na Mbunge huyo kwa kile alichokidai kuwa amekuwa na utovu wa nidhamu.

"Nimemuandikia barua Rais wa PAP ya kusitisha uwakilishi wake, hadi Kamati ya Maadili itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, na hapa kuna kamati mbili zinamsubiri ikiwemo Kamati ya Maadili ya Bunge na Kamati ya Maadili ya chama chake", amesema Ndugai.

Ndugai aliongeza kuwa, "Stephen Masele ni kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya hovyohovyo, ndiyo maana tumemuita atufafanulie huenda yuko sahihi, lakini anafanya mambo ambayo ni hatari kubwa, amekuwa akichonganisha mihimili miwili, ni amejisahau sana".

Mbunge huyo Masele amehukumiwa kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge kufuatia kosa lake hilo alilofanya.