Kiongozi wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al Burhan na mkuu wa kikosi maalumu cha jeshi kinachopambana na jeshi la taifa, RSF, Mohammed Hamdan Daglo, wamekubaliana juu ya mkataba wa usitishwaji mapigano kwa siku saba kuanzia Alhamisi Mei 4 hadi Alhamisi wiki ijayo Mei 11. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Sudan Kusini.
Taarifa hiyo imetolewa siku chache baada ya rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kuanza mazungumzo ya upatanishi kati ya pande hizo mbili zinazohasimiana, kama muwakilishi wa shirika la maendeleo la nchi za ukanda wa Afrika mashariki na pembe ya Afrika, IGAD. Kiir anatafuta kuyafikisha mwisho mapigano kati ya vikosi vya mkuu wa majeshi al Burhan na vile vya naibu wake Mohammed Hamdan Daglo anayekiongoza kikosi cha wanamgambo wa RSF.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Sudan Kusini imesema Al-Burhan na Daglo wamekubaliana kuwataja wawakilishi kwa ajili ya mazungumzo yatakayofanyika katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Wizara hiyo imesema hakuna terehe iliyopangwa ya lini mazungumzo hayo yatakapoanza, lakini hali ya kibinadamu inayozidi kuendelea kuwa mbaya inaifanya kuwa vigumu kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo. Makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano kwa saa 72 yameafikiwa tangu machafuko yalipozuka mnamo Aprili 15, lakini yamevunjwa mara kwa mara.