Alhamisi , 22nd Feb , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amefunguka na kuwashukuru Chama cha wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwa kuweza kutatua changamoto za wafanyakazi kwa kukaa nao mezani badala ya ule utaratibu wa zamani uliozoeleka wa kuandamana.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo

Gambo ameeleza hayo kupitia ukurasa wake maalumu wa kijamii asubuhi ya leo mara baada ya kupata taarifa ya mkoa wake kuchaguliwa kuwa wenyeji wa shughuli za Mei mosi kitaifa 2018.

"Tunawashukuru sana kwa kutupa heshima hii ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya muhimu yanayohusu wafanyakazi wetu. Nimewapongeza kwa utaratibu wenu wa kutafuta suluhu ya changamoto za wafanyakazi kwa kukaa mezani na serikali badala ya utaratibu wa kizamani wa kuandamana", amesema Gambo.

Sherehe za hizo zilizopewa jina la 'Sikukuu ya wafanyakazi' huwa zinaanzimisha kila ifikapo mwezi wa Tano tarehe moja nchini Tanzania ambapo Rais wa nchi huwa anatumia jukwaa hilo kutatua shida na kero za wafanyakazi papo kwa hapo pamoja na kutangaza kushusha au kupandisha daraja za mishahara bila ya kusahau kodi ya kichwa.