Jumatano , 28th Mei , 2014

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania imeitaka serikali kuhakikisha kuwa inapima, inachukua tahadhari pamoja na kuweka maandalizi ya kutosha ya kukabiliana na athari zinazoweza kutokana na uchimbaji wa madini ya urani.

Makamu mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu na utawala bora, Bi. Mahfoudha Hamid (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mstaafu Amir Manento.

Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Bi. Mahfoudha Hamid, amesema hayo leo jijini Dar-es-Salaam wakati utoaji wa chapisho linaloelezea madhara ya kiafya na mazingira iwapo Tanzania itaanza utekelezaji wa miradi ya uchimbaji wa madini ya urani.

Kwa mujibu wa Bi. Mahfoudha, taarifa za kisayansi zinaonyesha kuwa uchimbaji wa madini ya urani una madhara makubwa ya kiafya ikiwa ni pamoja na saratani za ini, mapafu, ubongo pamoja na mfumo wa uzazi.

Aidha, Makamu Mwenyekiti huyo wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora amesema uchimbaji wa madini ya urani pia unaathari kubwa za kimazingira ikiwa ni pamoja na kuhitaji maji mengi pamoja na kuchukua sehemu kubwa ya ardhi ambayo baada ya kumalizika shughuli za machimbo haiwezi kutumika tena.