Jumatano , 22nd Mei , 2019

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ametangaza kupangwa kwa miji katika maeneo yote itakapopita reli ya Mwendokasi (SGR), ili shughuli zitakazofanyika katika wilaya na vijiji inapopita reli hiyo kwenda sambamba na shughuli za kiuchumi za mradi wa reli hiyo.

Sehemu ya Reli ya kisasa ya (SGR).

Lukuvi amewatahadharisha wananchi wa vijiji hivyo, kutokubali kuanza kuuza maeneo yao kwa kuwa baada ya kupangwa kwa maeneo hayo, thamani ya ardhi itapanda na tayari baadhi ya watu wajanja kutoka nje ya vijiji hivyo washaanza kutafuta maeneo  kwa ajili ya fursa hiyo.

Waziri Lukuvi alisema hayo katika vijiji vya Kwala na Soga vilivyopo Kibaha mkoa wa Pwani alipozungumza na wananchi wa maeneo hayo, kuwaelezea mpango wa Wizara yake kupanga na kupima maeneo yote inapopita reli ya SGR ili kuendana na fursa za kiuchumi za mradi wa reli hiyo.

"Wilaya na vijiji vyote reli ya SGR itapita ardhi yao itapangwa na wale wananchi walio kando ya reli itakapopita, wasubiri  wasiwe na wasiwasi ardhi ya maeneo yao itengenezewe mpango na muongozo kuhusiana na maeneo hayo utatolewa" alisema Lukuvi.

Aidha, Lukuvi alisema wakati wa kupanga maeneo hayo hakuna mwananchi yeyote atakayenyang'anywa eneo lake, bali maeneo hayo yatapangwa kimji na kuainishwa matumizi yake kama vile ujenzi wa Viwanda na Mahoteli hivyo kuwataka wananchi wanaotaka kufanya uendelezaji mdogo mdogo kusubiri mpango huo.

Zaidi Tazama Video hapa chini.