Jumatano , 12th Feb , 2020

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Damas Ndumbaro, amesema kuwa Serikali haiwezi kuchukua jukumu la kuwaondoa Watanzania walioko nchini China kwa kusikiliza ushauri wa mitandaoni, bali itawaondoa endapo wataalamu kutoka Serikali ya China watashauri hivyo.

Watanzania waishio China wakiomba kurejeshwa nyumbani

Dkt Ndumbaro ameyabainisha hayo wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, baada ya kuonekana video fupi inayoonesha Watanzania waishio nchini China, wakiomba kurejeshwa nyumbani kutokana na hali ya maambukizi na vifo vinavyotokana na Virusi vya Corona kuongezeka kila uchwao nchini humo.

"Huu ni ugonjwa na hili ni suala la kitabibu hivyo ni vizuri kupata ushauri wa kitabibu, kwamba imefika wakati sasa hawa lazima waondolewe, sasa hivi tunasikia ushauri wa mitandaoni hapana, tukae na wataalamu wa Serikali ya China na waseme sasa hapa ni lazima kuwaondoa" amesema Dkt Damas Ndumbaro.

Mpaka sasa zaidi ya watu 1,000 wamekwishapoteza maisha kutokana na Virusi vya Corona, huku wengine zaidi ya 40,000, tayari wamekwishaathirika na virusi hivyo kwa Nchi ya China pekee.