Jumanne , 18th Jun , 2019

Shirika la umeme Nchini TANESCO limetekeleza agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Juni 13 Ikulu mara baada ya kukutana na wabunifu wa umeme kutoka mkoani Njombe la kuwataka kuwatembelea, kuwatambua, kuwapa ushauri wa kitalaamu.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco akimkabidhi pesa mmoja wa wabunifu

Wabunifu hao wamekabidhiwa fedha taslimu Sh. 5 milioni pamoja na hundi ya Sh. mil 10 kila mmoja huku lengo kuu likiwa ni kuthamini na kutambua ubunifu na jitihada ambazo zimechukuliwa na watu hao katika kutimiza ndoto zao.

Akizungumza mbele ya umati wa wakazi wa kijiji cha Lugenge wakati akikabidhi hundi ya fedha yenye thamani ya mil 10 pamoja na fedha taslimu mil 5 kwa wabunifu wote wawili akiwemo John Fute maarufu Dr. Pwagu na Laniel Ngailo Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dr. Titho Mwinuka amesema serikali itaendelea kuthamini na kutoa usaidizi wa kila hali ili kufikisha ndoto panapo stahili.

Kwa upande wao wabunifu hao wamesema imekuwa kama ndoto kwa Rais kutambua uvumbuzi na ubunifu wanaoufanya na kuamua kuwaunga mkono kwa kuwapa watalaamu na fedha ili kuboresha huduma zao huku pia wakionyesha hisia zao juu ya hatua ya TANESCO kuwakabidhi fedha taslimu mil 5 na hundi ya mil 10 kila mmoja kama ambavyo iliahidiwa.

Mara baada ya agizo naibu katibu mkuu, Mratibu wa masuala ya habari na maarifa kutoka COSTECH ndugu Deusdedith Lenard anasema agizo hilo litatekelezwa haraka iwezekanavyo kwa kuanza mara moja uboreshaji wa kiota hicho cha ubunifu kilichopo nyumbani kwa Pwagu ili kiweze kutumiwa na watu wengi kubuni vitu mbalimbali huku baadhi ya Wananchi wakizungumzia umuhimu wa Huduma ya Nishati ya Umeme.

Timu hiyo imewasili ikiwa na watalaamu kutoka TANESCO, COSTECH, REA, Wizara ya maji, Ewura na Mamlaka za Bonde la mto Rufiji na Nyasa huku kila mmoja akitazama namna ya kuwasaidia wabunifu hao ambao wamekumbana na changamoto nyingi mpaka kufikia hapo.