Jumatatu , 23rd Mar , 2015

Marais Uhuru Kenyetta wa Kenya na Jakaya Kikwete wa Tanzania wamekubaliana kufutilia mbali maagizo ya Tanzania kupunguza idadi ya ndege za Kenya zinazotua nchini na agizo la Kenya kupiga marufuku magari ya Tanzania kuingia katika uwanja wa ndege.

Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Jakaya Kikwete akiteta jambo na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Katika makubaliano hayo ndege za Kenya Airways sasa zitafanya safari zake kama kawaida nchini Tanzania na magari ya Tanzania yataruhusiwa kuchukua watalii na abiria katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta.

Akizungumza na waandishi wa habari waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernald Membe amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya viongozi hao wakuu wa nchi hizo mbili kukutana nchini Namibia walikokwenda kuhudhuria maadhimisho ya miaka 25 ya uhuru wa Namibia.

Makubaliano ya marais hao yanakuja siku chache baada ya mzungumzo ya mawaziri wa utalii wa Tanzania na Kenya kuvunjika mwishoni mwa wiki kufuatia pande hizo mbili kushindwa kufikia muafaka kuhusu magari ya Tanzania yaliyopigwa marufuku uwanja wa Jomo Kenyatta.