Jumamosi , 1st Aug , 2020

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), Hamza Johari, amesema kuwa sababu iliyopelekea na wao kuzizuia Ndege za Kenya kutua nchini ni baada ya nchi hiyo kuzuia ndege za Tanzania kutua kwao na kuongeza kuwa hali ya namna hiyo ni kawaida katika biashara.

Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, James Macharia na kulia ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Anga nchini, Hamza Johari.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 1, 2020, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya Eats Africa Radio na kuongeza kuwa, nchi ya Kenya ilikuwa imeomba ruhusa ya Ndege zake kutua nchini kuanzia leo, lakini wao walishangazwa kuona Kenya yenyewe imezuia ndege za Tanzania hivyo na wao wakaamua kuchukua maamuzi ya sawa kwa sawa.

"Tumefikia uamuzi huo kwa sababu katika sheria na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa usafiri wa anga kati ya nchi na nchi ni kwamba, Mataifa yanatakiwa yawe sawa kwa sawa, Kenya walikuwa wameomba kuja Tanzania kuanzia leo kutua katika viwanja vya Dar es Salaam, Zanzibar na Kilimanjaro na sisi hatukuwa na tatizo tukawapa ruhusa, lakini baadaye tukasikia wao wanatuzuia sisi tusiende kule" amesema Johari.

Aidha Mhandisi Hamza ameongeza kuwa "Mwaka 2015 walizuia gari za watalii zisiingie Kenya, kwahiyo tukafanya hivyo na baada ya siku mbili wao wakaondoa kikwazo walichotuwekea, tumetendewa kitu ambacho si sahihi na sisi inabidi tufanye hivi badala ya kukaa kimya na kuwaacha wao waendelee kufanya wanachotaka".

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema kuwa siku ya Jumanne kutakuwa na mkutano na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili wajue nini chanzo kilichopelekea nchi ya Kenya kuzuia Ndege za Tanzania zisitue nchini humo.

Aidha East Africa Radio ilimtafuta Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, James Macharia, ambaye alikataa katakata kama nchi yao imezuia Ndege za Tanzania kutua nchini humo.

"Hakuna ndege ya Tanzania ambayo imezuiliwa kuingia Kenya, sisi tulisema hizo nchi tulizoziweka kwenye hiyo orodha watu wao wakifika hapa hawatakaa karantini, lakini kama nchi haipo kwenye hiyo orodha watawekwa Karantini, sisi taarifa ya kuzuiwa kuingia Tanzania tumeipata lakini tutazungumza na wenzetu na tutasikilizana" amesema Waziri wa Kenya.