Jumatano , 11th Nov , 2015

Tanzania imetajwa kuwa nchi pekee barani Afrika kuwa na vivutio vingi vya uwekezaji, sifa inayoiweka kwenye mazingira mazuri ya kuendelea kiuchumi kutokana na idadi kubwa ya wawekezaji kuja kuwekeza nchini.

Bw. Lin Zhiyong kutoka China akisalimiana na Rais wa Chama Cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda Tanzania (TCCIA) Bw. Aloys Mwamanga.

Hayo yamezungumzwa na mkuu wa kitengo cha uchumi na biashara kwenye ubalozi wa China nchini Tanzania Bw. Lin Zhiyong kwenye uzinduzi wa kampuni ya kutengeneza na kuuza mashine za ujenzi ya AVIC-SHANTUI.

Zhiyong amesema Tanzania imechaguliwa na China kuwa sehemu ya kuwekeza kutokana na sifa zake kubwa ikiwemo amani na utulivu hasa ambayo imethibitika baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu mwaka huu.

Ameongeza kuwa tofauti na hali ya amani pia Tanzania imebarikiwa kuwa na malighafi ikiwemo chuma, gesi asilia na rasimali nyingine ambazo kwa namna moja au nyingine zinawavutia wawekezaji hasa kutoka nchini China.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uledi Musa amesema nia ya serikali ni kutumia viwanda na biashara kukuza uchumi na kuongeza kuwa ugunduzi wa chuma cha liganga na makaa ya mawe ni hazina kubwa kwa taifa.

Aidha Lin amesema kuwa China inaendelea kujipanga kuwa kiongozi wa uchumi duniani ikiyapiku mataifa mengine ya Ulaya na Marekani kwani wawekezaji wa taifa hilo wanatafuta maeneo muhimu yenye mvuto wa kibiashara ambapo Tanzania imepewa kipaumbele.