Jumapili , 17th Aug , 2014

Kundi la Tembo limevamia makazi ya wananchi wa kata ya Tingatinga wilayani Longido mkoani Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kujeruhiwa.

Wakazi wa Longido wakigawana nyama ya Tembo kwa ajili ya kitoweo

Kundi la Tembo limevamia makazi ya wananchi wa kata ya Tingatinga wilayani Longido mkoani Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kujeruhiwa.

wananchi wa kata hiyo wameiambia EATV kuwa aliyeuawa na Tembo hao ni mtoto wa miaka Tisa aliyetajwa kwa jina la Fred Joseph na Bw Paulo Lukasi ambaye amejeruhiwa na kulazwa hosipitalini.

Wakizungumza baada yakikosi cha kuzuia ujangili kanda ya kaskazini kufika na kushirikiana nao kumuua tembo aliyesababisha madhara hayo wananchi hao wamelalamikia watendaji wa sekta ya wanyamapori kwa kuendelea kukaa mijini na kusubiri kupewa taarifa wakati wananchi vijijini wakiendelea kuuawa.

Diwani wa kata ya Tingatinga Bw, Sabore Olemoloimet ameiomba serikali kuhakikisha watendaji wanaoshughulikia migogoro ya wananchi na wanyamapori kuhamia maeneo husika ili waweze kuwadhibiti wanyama kabla hawajaleta madhara.

Mkuu wa wilaya ya Jongido Bw James Olle Millya amekiri kuwepo kwa udhaifu mkubwa kwa watendaji wanaoshughulikia wanyamapori na kwamba licha ya kutoa maelekezo mara kadhaa bado hayafanyiwi kazi.

Baada ya Tembo huyo kuuawa makundi ya wananchi wa eneo hilo yalifika na kuanza kumgawana kwa ajili ya kitoweo huku wakimshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuondokana na tatizo hilo na pia kupata kitoweo.

Vilio vya wananchi juu ya madhara yanayosababishwa na wanyamapori wakiwemo Tembo vimekuwa vikisikika katika kona mbalimbali nchini jambo linaloonyesha kuwa bado tatizo hilo halijapata ufumbuzi wa kudumu