Jumatatu , 1st Sep , 2025

"Idadi ya vifo na majeruhi ni kubwa, lakini kwa kuwa eneo hilo ni gumu kufikiwa, timu zetu bado ziko eneo la tukio," msemaji wa wizara ya afya Sharafat Zaman amesema katika taarifa.

Mamia wanahofiwa kufariki na wengine kujeruhiwa katika tetemeko la ardhi la kipimo cha 6 lililokumba mkoa wa kaskazini-mashariki mwa Afghanistan wa Kunar, mamlaka imesema leo Jumatatu Septemba Mosi, wakati waokoaji wakifukua vifusi vya nyumba katika kuwasaka manusura.

Ripoti za awali kutoka wizara ya afya nchini humo zimeonyesha kuwa watu 30 wamekufa katika kijiji kimoja, lakini takwimu sahihi za majeruhi bado hazijakusanywa katika eneo la vijiji vilivyotawanyika kufuatia historia ndefu ya matetemeko ya ardhi na mafuriko.

"Idadi ya vifo na majeruhi ni kubwa, lakini kwa kuwa eneo hilo ni gumu kufikiwa, timu zetu bado ziko eneo la tukio," msemaji wa wizara ya afya Sharafat Zaman amesema katika taarifa.

Mamia ya waliojeruhiwa wamepelekwa hospitalini, kwa mujibu wa Najibullah Hanif, mkuu wa habari wa mkoa, na huenda takwimu zikaongezeka kutokana na ripoti kuwasili kutoka maeneo ya mbali yenye barabara chache.

Waokoaji wamekuwa wakifanya kazi katika wilaya kadhaa za mkoa huo wa milimani ambapo tetemeko hilo la usiku wa manane lilipiga kwa kina cha kilomita 10 (maili 6), na kusawazisha nyumba za udongo na mawe kwenye mpaka na mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa wa Pakistan, maafisa wamesema.

Afghanistan inakabiliwa na matetemeko mabaya ya ardhi, haswa katika safu ya milima ya Hindu Kush, ambapo mabamba ya mwamba ya Hindi na Eurasia hukutana. Msururu wa matetemeko ya ardhi magharibi mwake yaliua zaidi ya watu 1,000 mwaka jana, na kusisitiza hatari ya moja ya nchi masikini zaidi duniani kwa majanga ya asili.