Alhamisi , 23rd Mei , 2019

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro amesema kuwa maeneo ya viwanja vya ndege ususan kiwanja cha ndege Dar es salaam kamwe hakitakuwa uchochoro wa kupitisha na kusafirisha magendo, biashara ya binadamu, nyara za serikali pamoja na dawa za kulevya.

IGP, Simon Sirro (katikati) alipotembelea Uwanja wa Ndege wa JNIA

IGP Sirro ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya ukaguzi katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) terminal III kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho ambacho hadi sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99.

Amesema kuwa, Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha hali ya usalama inakuwepo kiwanjani hapo na kwamba hakuna mtu atakaye jaribu kuutumia uwanja mpya wa ndege terminal III kwa vitendo vya kuhujumu uchumi wa taifa.

Naye Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha JuliusNyerere (JNIA), Paulo Rwegasha, amesema kuwa, wameendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu vinavyotokea kiwanjani hapo na kwamba hadi sasa kutokana na ushirikiano uliopo wamefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa uhalifu.

Wakati huo huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro, amefanya ziara ya ukaguzi katika kikosi cha kutuliza ghasia FFU Ukonga Dar es salaam na kuzungumza na maofisa na askari wa vyeo mbalimbali ambapo katika ziara yake amewapandisha vyeo askari wawili kuwa sargent na koplo wa Polisi kutokana na umahiri wao na kujituma kazini.