Jumatatu , 31st Aug , 2015

Chama cha ACT-Wazalendo jana kimezindua kampeni zake za urais, wabunge na madiwani kwa nchi nzima katika viwanja vya Zakhiem jijini Dar es Salaam huku wakiweka vipaumbele vinne katika ilani yao kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa.

Mgombea Urais Kupita chama cha ACT-Wazalendo Anna Elishia Mghwira akihutmia mamia ya Wananchi waliojitokeza katika siku ya Uzinduzi wa Kampeni ya Chama hicho

Akizungumza na Mamia waliojitokeza katika viwanja hivyo Mgombea Urais kupitia chama hicho Mama Anna Elishia Mghwira amesema vipaumbele katika ilani yao ni poamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Uchumi Shirikishi, Kilimo pamoja na Elimu huku akielezea mikakati waliyoipanga katika kutekeleza sera hizo.

Anna amesema serikali yake itatengeneza sera ya uchumi shirikishi ambayo kilimo kitatumika kama sekta muhimu ya kuinua uchumi wa nchi pamoja kuondoa umasikini.

Ameongeza kuwa wakulima wamekuwa hawana masoko ya kueleweka na kukosa kupata faida kutokana na mazao yao.

Bi. Anna amesema serikali yake itafufua uchumi wa viwanda ikiwemo viwanda vya pamba ambavyo vitatumika katika kutengenezea nguo ambayo ni malighafi yenye soko kubwa nchini Tanzania hivyo kuwakomboa wakulima wengi kutoka katika lindi la umsikini.

Kwa upande wake kiongozi wa chama hicho Mh. Zitto Zuberi Kabwe amesema ACT ndiyo chama pekee chenye nia ya dhati ya kupambana na rushwa na ndio misingi waliyojiwekea ikiwa ni katika kurudisha uongozi katika misingi ya maadili.

Aidha Mh. Zitto amesema Chama cha Mapinduzi na UKAWA havijaonesha nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi kutokana na sera zao kutotangaza ni jinsi gani wataweza kupata pesa za kutekeleza ahadi zao.

Naye upande wake Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa watanzania wanataka kiongozi wa nchi na sio afisa miradi kauli ambayo ameitoa kutokana na Mh. Fredrick Sumaye katika uzinduzi wa kampeni za UKAWA kufananisha cheo cha Rais kuwa sawa na meneja.