Jumapili , 20th Mar , 2016

Wananchi wa Zanzibar leo wanapiga kura katika uchaguzi wa marudio wa rais, madiwani na wawakilishi, uchaguzi unaofanyika baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC kufuta ule wa Oktoba 25 mwaka jana kwa madai ya kuwepo kwa kasoro nyingi.

Orodha ya wagombea wa nafasi ya urais kama ilivyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar - ZEC.

Mwandishi Wetu Noah Laltaika ambaye yupo Kisiwani Zanzibar kwa ajili ya kutuletea kinachoendelea katika uchaguzi huo amesema mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Ali Mohamed Shein, amepiga kura yake katika kituo kilichopo shule ya msingi ya Bungi jimbo la Kibele mkoa wa Kusini Unguja majira ya saa moja na dakika tano mapema hii leo.

Viongozi wengine wakuu wa kitaifa wakiwemo wastaafu wamejitokea kushiriki haki yao ya kidemokrasia, kati yake yumo Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa rais Bi. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Akizungumza mara baada ya kupiga yake, Dkt. Shein amesema kuwa kwa ujumla kumekuwa na hali ya utulivu visiwani humo na kwamba ni mategemeo yake hali itakuwa hivyo katika maeneo yote kwani usalama umeimarishwa.

Katika maeneo mengi kumekuwa na taarifa za idadi ndogo ya watu waliojitokeza ingawa katika vituo vingi wanawake ndio wamekuwa wengi na kuonyesha muitikio mkubwa wa kushiriki haki yao hiyo ya kidemokrasia.

Uchaguzi huo unafanyika licha ya chama kikuu cha upinzani cha Civic United Front (CUF) na vyama vingine kadhaa, kususia kwa madai ya kutotambua sababu zilizopelekea Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana.