Ufaulu wa Mwanafunzi Anna aliyefiwa na wazazi

Ijumaa , 10th Jan , 2020

Mwanafunzi Anna Zambi ambaye wazazi wake walifariki wakati wakienda kwenye mahafali yake mkoani Tanga, amefaulu kwa kupata daraja la 1 (Division 1 ya 14), katika matokeo ya kidato cha 4 yalitolewa jana.

Mwanafunzi Anna Zambi

Anna Zambi alimaliza Kidato cha 4 katika Shule ya Sekondari ya Mather Theresia of Calata iliyopo mkoani Kilimanjaro.

Mara baada ya kuwazika wazazi wake Waziri Ummy aliandika kuwa "hili jambo ni kubwa mno kwa mtoto Anna Zambi, inaumiza sana ninamuombea kwa Mungu ampe nguvu na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu, kama mzazi na Waziri mwenye dhamana ya Ustawi na Maendeleo ya Watoto nami nitamfikia Anna kwa ajili ya kumfariji na 'support' nyingine." alisema Waziri Ummy.

Wazazi wa Anna walikuwa wakifahamika kwa majina ya Lingston Zambi na Winifrida Lyimo na wadogo zake watatu, Lulu, Andrew na Grace waliaga Dunia katika ajali hiyo baada ya gari walilokuwa wamepanda kusombwa na maji, kutokana na mvua kubwa iliyonyesha wilayani Handeni mkoani Tanga.