Ijumaa , 2nd Sep , 2016

Uwekezaji katika ufugaji wa samaki sambamba na kilimo mchanganyiko umetajwa kuwa moja ya fursa chache ambazo iwapo itaungwa mkono na serikali inaweza kuwa suluhisho la kiuchumi kwa idadi kubwa ya Watanzania

Wajasiriamali Abdul Omary Kamugisha na Petro Nyaruba wakionesha moja ya samaki kutoka katika bwawa lao.

Suluhisho hilo linaweza kutimiza ndoto za serikali za kulivusha taifa kuwa la uchumi wa kati.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na wajasiriamali wawili, Bw. Abdul Omary Kamugisha na mwenzake Petro Nyaruba Maguge, ambao kupitia mradi wao Boko Fish Farming ulioanza Januari mwaka huu, wameweza kufuga samaki ambao mpaka kufikia mwezi ujao, wanatarajia kuvuna takribani tani hamsini za samaki watakaowaingiza sokoni na hivyo kupunguza uhaba wa kitoweo cha samaki nchini.

Aidha, wajasiriamali hao wametaja changamoto inayowakabili kuwa ni uhaba wa fedha na kwamba iwapo watapata udhamini wa serikali, wana uwezo wa kujenga mabwawa hamsini ya samaki, yatakuwa na uwezo wa kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya mia mbili kama anavyoeleza katika mahojiano na EATV iliyotembelea eneo la Kigamboni ambako mradi huo unatekelezwa.