Jumanne , 22nd Oct , 2019

Kufuatia kuwepo kwa malalamiko ya upungufu wa walimu katika maeneo ya vijijini mkoani Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loatha Ole Sanare amepiga marufuku walimu waliopo maeneo ya vijijini kuhamishiwa manispaa ya Morogoro bila kufuata utaratibu.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Loatha Ole Sanare.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo hilo  kwenye kikao kilichowakutanisha Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa halmashauri pamoja na maafisa taaluma wa halmashauri zote mkoani humo, ambapo amesema kuwa hali hiyo ni moja ya sababu inayochangia baadhi ya shule kufanya vibaya kutokana na upungufu wa walimu.

Ole Sanare ameongeza kuwa, uhamisho usiofuata taratibu umechangia kuwepo kwa upungufu mkubwa wa walimu kwenye shule za msingi na sekondari zilizopo kwenye maeneo hayo.

Aidha Mkuu wa Mkoa Ole Sanare amesema kuwa amepata taarifa ya kutokuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya ofisi za kitendaji mkoani hapa hivyo  amewataka watendaji kushirikiana ili kutatua changamoto zilizopo.

Kwa upande wao baadhi ya watendaji kwenye halmashauri mkoani hapo wamesema kuwa kuna baadhi ya shule zilizopo maeneo ya vijijini zina walimu wachache, hivyo maagizo ya Mkuu wa Mkoa yatasaidia kuboresha sekta ya elimu mkoani Morogoro.