Jumanne , 3rd Feb , 2015

Rais wa Jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck ameanza ziara yake ya siku tano nchini Tanzania leo ambapo amepokewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete huku wakikubaliana kuboresha sekta mbalimbali.

Rais wa Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha mgeni wake Ikulu Rais wa Ujerumani Mhe. Joachim Gauck ambaye ameongozana na mke wake Bibi schadt leo Tarehe.03.02.2015

Rais wa Jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck ameanza ziara yake ya siku tano nchini Tanzania leo ambapo amepokewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete huku wakikubaliana kuboresha sekta mbalimbali nchini hususani ya biashara.

Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam Rais katika mazungumzo na waandishi wa Habari mara baada ya kufanya mazungumzo ya faragha, Dkt. Jakaya Kikwete ameiomba serikali ya Ujerumani kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya sekta ya gesi, Viwanda pamoja na Biashara ili kukuza uchumi huku akisisitiza kuwa mahusiano ya kisiasa na kijamii kati ya Tanzania na Ujerumani yamezidi kuimarika.

Akitoa taarifa ya makubaliano waliyoafikiana, Rais Kikwete amesema kuwa Rais wa Ujerumani Joachim Gauck amesema kuwa Ujerumani iko tayari kuongeza uwekezaji kutoka miradi iliyopo sasa ambapo kwa sasa Ujerumani ina miradi 151 ya kiuchumi yenye thamani ya takriban Euro Milion 300 karibu Bilion 621 za kitanzania

Rais Kikwete amesema kuwa msisitizo zaidi ameuweka katika uwekezaji kwenye sekta ya gesi ambayo endapo itafanikishwa kuenea Tanzania itasaidia kuondoa tatizo la uharibifu wa misitu akitolea mfano wa Jiji la Dar es Salaam ambalo hutumia zaidi ya tani elfu 40 za mkaa kwa mwaka.

Kwa upande wake Rais Joachim Gauck amesema kuwa Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania kibiashara na Kiuchumi na ndiyo maana katika msafara wake ameongozana na wadau mbalimbali wa sekta za kiuchumi kutoka Ujerumani wakiwemo wafanyabiashara wakubwa na waziri husika kwa lengo la kujifunza na kuangalia fursa za uwekezaji.

Rais Gauck ameongeza kuwa anaridhishwa na jinsi Tanzania inavyosimamia haki za binadamu pamoja na kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa, umoja wa kitaifa na maendeleo na kwamba Ujerumani itaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo na Tanzania.

“Tuko hapa kwa ajili ya kujifunza na kuangalia namna ya kusaidiana kiuchumi na kuimarisha biashara baina ya Ujerumani na Tanzania” Amesema Rais Gauck

Amesema “Ujerumani na Tanzania zimekuwa na ushirikiano mkubwa wa kihistoria tangu mwaka 1961 na ndiyo maana kuna shule, makanisa n.k vilivyojengwa na wajerumani.... na pia imekuwa ikiisaidia Tanzania kifedha”

Ameipongeza Tanzania kwa kushiriki kikamilifu katika jitihada za kutafuta amani katika mataifa mbalimbali ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kama vile Sudani Kusini na DRC.

Wakijibu maswali ya waandishi wa Habari, Rais Kikwete amejibu swali lililohusu mgogoro wa mpaka katika ziwa Nyasa ambapo amesema kuwa mgogorohuo unaendelea kushughulikiwa.

Swali lingine lilihusu hali ya Uhuru wa vyombo vya habari ndani ya Tanzania kufuatia kufungiwa kwa gazeti la The East African, pamoja na kitendo cha askari kuwapiga wafuasi wa CUF waliokuwa wakiandamana January 27 mwaka huu.

Akijibu maswali hayo Rais Kikwete amesema “Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zinajali sana uhuru wa vyombo vya habari na hata sasa kuna magazeti mengi yaliyosajiliwa na yanafanya kazi zake kwa uhuru”

Kuhusu kufungiwa kwa gazeti la The East African Rais Kikwete amesema suala hilo linashughulikiwa na mamlaka husika kwa sheria na taratibu stahiki za usajili wa magazeti.

Kuhusu kupigwa kwa wafuasi wa CUF amesema kuwa wafuasi wale akiwemo mwenyekiti wao Prof Ibrahim Lipumba hawakufuata taratibu za kukusanyika ndiyo maana yalitokea yaliyotokea.

“Kwa Tanzania tuna taratibu zetu za vyama vya siasa kukusanyika, wala hatubani haki na uhuru wa wapinzani... tena wapinzani wanafanya mikutano mingi zaidi kuliko chama tawala.... lakini ikitokea hawajafuata taratibu, hatuwezi kuwaacha waendelee kuvunja sheria na taratibu”

Kuhusu hali ya usalama na tishio la ugaidi, Rais Kikwete amesema kuwa anatambua kuwa Tanzania haiwezi kujiamini kwa asilimia 100 kuwa iko salama na haitakumbwa na vitendo hivyo, lakini ana imani kuwa kiwango cha usalama ni kikubwa na kwamba Tanzania ina uzoefu na matukio hayo ikikumbukwa tukio la ulipuaji wa ubalozi wa Marekani ambapo baadhi ya waliohusika walikuwa ni wafuasi wa kundi la Al Shabaab.

“Mara kwa mara tupo katika tahadhari ya tishio hilo, na bahati nzuri tunashirikiana vizuri na vyombo vya usalama vya kimataifa vikiwemo vya Ujerumani kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa salama lakini si salama kwa asilimia 100” amesema Rais Kikwete

Kwa upande Rais Gauck ameipongeza Tanzania na kusema kuwa ni mfano wa kuigwa kwa jinsi inavyojituma kupeleka majeshi yake katika mataifa yenye machafuko, kwani kwa kufanya hivyo inajilinda yenyewe.

Rais Gauck anatarajiwa pia kutembelea Zanzibar, Bagamoyo, hifadhi ya Taifa ya Serengeti na ameomba akae Arusha kwa muda kabla ya kurejea Ujerumani.