UTAFITI TWAWEZA, KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015

Jumatano , 12th Nov , 2014

Mwananchi mmoja kati ya watatu (33%) Tanzania Bara hajui ni nani atayekuwa chaguo lake la Rais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Hakuna mgombea hata mmoja anayependwa na wapiga kura kwa zaidi ya 15%.

Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na Twaweza mwezi Septemba 2014, anayeongoza ni Edward Lowassa (13%) akifuatiwa na Mizengo Pinda (12%) wote wa CCM, na watatu ni Dkt. Wilbrod Slaa wa Chadema (11%). Wafuasi wa CCM walipohojiwa, robo yao (24%) walisema watampigia kura yeyote atakayeteuliwa na chama.

Ukilinganisha kukubalika kwa vyama, nusu ya Watanzania (51%) wanasema wataipigia kura CCM kwenye uchaguzi wa Rais, na robo moja ya Watanzania (23%) wataipigia kura Chadema. Walipoulizwa watafanya nini kama vyama vya upinzani vitaungana na kusimika mgombea mmoja tu, kama UKAWA ilivyoahidi kufanya, CCM bado inaongoza lakini idadi ya watakaoichagua CCM inapungua hadi chini ya nusu (47%) ya wananchi wote. Wakati huohuo, karibu wananchi watatu kati ya kumi (28%) wamesema wangempigia kura mgombea wa upinzani. Idadi kubwa ya wananchi, mmoja kati ya watano (19%) amesema hatapigia kura chama bali mgombea. Ikitokea kundi hili likaamua kumpigia kura mgombea wa upinzani, ushindani utakuwa mkali mwaka 2015.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Tanzania kuelekea 2015: Maoni na matakwa ya wananchi juu ya uongozi wa kisiasa. Muhtasari huu umetokana na Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu ya mkononi maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar haimo kwenye matokeo haya). Matokeo muhimu yametokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,445 mwezi Septemba 2014.

Linapokuja suala la upenzi wa vyama, ukweli uko wazi, CCM inaendelea kuwa na wafuasi wengi zaidi kuliko vyama vingine. Wahojiwa walipoulizwa wangependa kumpigia kura mgombea wa chama gani kwenye nafasi za Rais, Mbunge au Diwani, CCM inaongoza kwa mbali. Karibu mara mbili ya idadi ya wahojiwa wanasema watawachagua wagombea wa CCM kwa nafasi hizi, ikilinganishwa na mpinzani wake Chadema. Vile vile 54% ya walioshiriki kwenye utafiti wa Sauti za Wananchi wanasema kuwa wao ni wafuasi wa CCM, wakati wahojiwa 27% walijitambulisha kuwa ni wafuasi wa Chadema.

Hata hivyo, hali hii inaweza isiendelee kutokea, CCM imekuwa ikipoteza kura zake tangu mwaka 2005, Mathalani, kura za CCM zilishuka kutoka 80% (2005) hadi 61% (2010) na mwaka 2014 zimeshuka hadi 54%. Kwa mujibu wa takwimu za Twaweza). Aidha upenzi wa vyama ukiangaliwa kwa umri kuna ukweli ulio wazi kuwa Chadema inapendwa zaidi na wapiga kura vijana. Miongoni mwa wananchi wenye umri chini ya miaka 35, 44% wamedai ni wafuasi wa CCM, wakati 34% wanaunga mkono Chadema. Hii inaweza kutofautishwa na upenzi wa vyama, wananchi wenye umri kati ya miaka 35- 50 ambao ni 60% wanaiunga mkono CCM na 24% wanaiunga mkono Chadema. Kama hali hii haitabadilika, Chadema inaweza kuongeza kura zake katika siku zijazo.

Kwa ujumla, wananchi pia wamechoka kudanganywa katika masuala ya kisiasa na wawakilishi wao waliowachagua. Walipoulizwa kama wanao mpango wa kuwachagua tena wabunge wao, karibu nusu ya wananchi (47%) walisema hawatawachagua tena. Pengine ni kwa sababu wananchi hawaoni kama wabunge wao wanatimiza ahadi zao. Wananchi nane kati ya kumi (79%) wameripoti kuwa wanakumbuka ahadi zilizotolewa na wabunge wao wakati wa kampeni uchaguzi uliopita, na wananchi watatu kati ya kumi (32%) wamesema wabunge wao hawajatimiza ahadi yoyote kati ya yale waliyoyaahidi. Wananchi 16% wameripoti kuwa mbunge wao ametimiza ahadi chache. Hata hivyo, wanne kati ya kumi (38%) wameripoti kufuatilia ahadi kwa mbunge wao. Kwa ujumla, ni wananchi wenyewe waliosema kuwa wabunge wao wametekeleza ahadi chache au hawajatekeleza ahadi hata moja, kitu kilichowafanya waripoti kuwa hawatawachagua tena wabunge hao.

Kwa kuangalia takwimu za utafiti wa Sauti za Wananchi, kushuka kwa uaminifu na ushiriki kwenye uwanja wa kisiasa kumeonekana kuendelea. Mwaka 2012, hakuna mwananchi hata mmoja aliyesema angempigia kura mgombea na sio chama. Lakini mwaka 2014, wastani wa wahojiwa 17% wamesema hawatachagua chama bali mgombea kwenye uchaguzi wa udiwani, ubunge na hata urais. Lakini ishara kubwa ya kutoridhika inatokana na viwango vya uaminifu vilivyoripotiwa kuhusu ofisi husika. Kwa nafasi zote, kuanzia Rais, wabunge hadi wenyeviti wa mitaa / vijiji, wananchi wana imani ndogo na watendaji wanaoshikilia nafasi hizo leo kuliko miaka miwili iliyopita. Imani ya wananchi imepungua sana kwa wenyeviti wa mitaa / vijiji na madiwani ambao viwango vya kukubalika vimeshuka kwa 25% (mwenyekiti wa kijiji / mtaa) na kwa 23% (madiwani). Imani kwa Rais pia imepungua kutoka 45% mwaka 2012 hadi 31% mwaka 2014.

Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alibainisha: "Uchaguzi wa vyama na viongozi unahakikisha wananchi wanasikilizwa. Takwimu zinaonesha kuwa, watu kwa ujumla wanaona kuna tatizo kwenye utekelezaji wa sera, na kushughulikia masuala muhimu kama vile umaskini, elimu na afya. Wengi hawaridhiki na utendaji kazi wa wabunge wao na hawatawachagua tena. Na miongoni mwa wagombea wa urais, hakuna mgombea anayeaminika wa kutosha, uwanja wa ushindani uko wazi. Kati ya vyama vyenye wafuasi wengi CCM bado inaongoza, lakini sehemu ya kura zake zimepungua, na inaweza kutishwa zaidi kama kura za watu ambao bado hawajaamua zitakwenda kwa umoja wa upinzani. "

"Kwa kifupi", aliongeza Rajani "inaonekana kuwa wananchi wengi wanataka utekelezaji na uongozi imara. Wagombea wa kisiasa watafanya vizuri kusikiliza watu na kushughulikia vipaumbele vya wananchi kwa njia zinazoeleweka na zenye kufikia mafanikio."
Message 31 of 32