Ijumaa , 28th Oct , 2016

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Crispin Kahesa amesema watanzania wengi  hawana utamaduni kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kubaini kama kuna dalili zozote za  magonjwa ili yaweze kutibiwa mapema.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Crispin Kahesa

 

Akizungumza Jijini Dar es salaam katika kipindi cha EAST AFRICA BREAKFAST cha EATV,  Dkt. Kahesa amesema wagonjwa wengi wa saratani hufika hospitalini wakiwa wameshaathirika kwa kiasi kikubwa wakati wangefika mapema wangeweza kutibiwa na kupona kabisa au kuanza matibabu mapema.

“Utamaduni ni kikwazo kikubwa kwa wananchi kupima afya zao, ni vyema watanzania tujenge utamaduni wa kupima afya zetu mapema ili kuweza kujikinga na maradhi mapema la sivyo hali siyo nzuri hata kidogo” Amesema Dkt. Kahesa.

Aidha Dkt. Kahesa amesema ugonjwa wa saratani umeshamiri sana  kwa sasa kutokana na ongezeko la watu pamoja na mfumo wa maisha ya kila siku huku akisema kuwa saratani inayoongoza ni saratani ya shingo ya kizazi kwa kina mama.