
Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam inatarajiwa kutoa uamuzi wake juu ya picha mjongeo (video) ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu iliyopokelewa mahakamani hapo kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili mshtakiwa huyo, kujulikana leo.
Uamuzi huo unatarajia kutolewa leo Jumatano Oktoba 22, 2025 ukilenga kutoa taswira ya jumla ya kesi hiyo kwa kuamua ni nani mshindi kufuatia video hiyo yenye hoja zinazodaiwa kuwa na maudhui (maneno) ya uhaini yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kutishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde katika hatua ya ushahidi wa Jamhuri, ikiwa ni shahidi wa tatu.
kesi ya Lissu inatokana na maneno aliyoyatoa mnamo mwezi Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, yanayodaiwa kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii akisema kuwa:
"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli..., kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko..., kwa hiyo tunaenda kukinukisha..., sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana...".