Jumatatu , 22nd Mei , 2023

Wakazi wa Kijiji cha Sunuka Uvinza mkoani Kigoma, kwa kushirikina na serikali ya kijiji hicho, wamelazimika kuchukua waganga wa jadi zaidi ya 10 kutoka Sumbawanga ili kukagua watu wanaofanya uchawi wakidai kuwa chanzo cha vifo vya vijana katika mazingira ya kutatanisha.

Wananchi wa kijiji cha Sunuka

Waganga hao wamepewa dhamana hiyo ya kusaka wachawi kijijini hapo ambapo wananchi waliandamana hadi mpakani mwa kijiji cha Rulinga kuweka vizuizi kwa Mkuu wa wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani asiingie katika kijiji Chao wakihofia atazuia oparesheni hiyo. 

Katika mkutano huo Mkuu wa wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani ametoa maelekezo ambayo yamekataliwa na wananchi, kwa madai kuwa suala hilo halipo kisheria na hata serikali haiamini licha ya wananchi wakihitaji atoe kibali cha kuendelea na zoezi hilo la kusaka wachawi .

Hatua ya kukosekana makubaliano, inailazimu kamati ya usalama kurudi nyuma vijiji viwili hadi Ilagala na kujadili suala hilo kisha kutoa tamko rasimi ambapo Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, ameagiza waganga hao waondoke mara moja la sivyo sheria itawahusu wakiwepo pia viongozi wanaotoa kibali cha kusaka wachawi.

Tetesi zinasema, ili kufanikisha zoezi hilo, wananchi wanachangishwa shilingi elfu tano kuwezesha oparesheni hiyo, ikipata baraka kutoka serikali ya kijiji, licha ya viongozi wa Kijiji akiwemo mwenyekiti Hamisi Idi na Diwani hawakuweza kutokea katika mkutano.