Idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko kubwa la ardhi lililotikisa Afghanistan imeongezeka hadi 1,411, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu la Afghanistan (Afghan Red Crescent Society).
Shirika hilo la kibinadamu limesema pia zaidi ya watu 3,124 wamejeruhiwa na zaidi ya nyumba 8,000 zimeporomoka kutokana na tetemeko hilo.
Katika mkoa wa Kunar, ambako ndiko kitovu cha tetemeko hilo lenye ukubwa wa kiwango cha 6, waokoaji wanafanya juhudi za kufika vijiji vya milimani ambavyo bado havijafikiwa.
Kwa mujibu wa Ehsanullah Ehsan, mkuu wa idara ya usimamizi wa majanga mkoani humo, operesheni za uokoaji zimekamilika katika vijiji vinne na sasa zinalenga maeneo yaliyo mbali zaidi.
Changamoto kubwa inayokwamisha juhudi za uokoaji ni barabara nyembamba za milimani na hali mbaya ya hewa, ambazo zimezuia magari kufika maeneo yaliyoathirika. Mashine maalum zimesafirishwa ili kuondoa kifusi barabarani na kurahisisha upatikanaji wa huduma za msaada.

