Jumapili , 1st Dec , 2019

Mwenyekiti wa Baraza la watu wanaoishi na Ukimwi hapa nchini (NACOPHA), Leticia Kapela, amewataka vijana kujiepusha na ngono isiyo salama, sanjari na kuwaonya vijana wanaopenda kujihusisha kimapenzi na watu wazima hii ni kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la vijana wanaoishi na ugonjwa

Hayo ameyabainisha leo Desemba 1, 2019, Jijini Mwanza, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani na kuwataka wanaume watu wazima, wanaowarubuni mabinti kuingia nao katika mahusiano ya kimapenzi waache tabia hiyo.

"Vijana tutumie kinga sababu nikisema watu muache hamuelewi kabisa, acheni ngono, kwani lazima ufanye? mmeambiwa hicho ni chakula ambacho ukiacha kukila utapata Utapiamlo?, lakini pia kuna tabia ya vijana wadogo kuomba kulelewa na wanawake watu wazima kama mimi, unakuta kijana anakufuata anaomba umlee unamuuliza kwani wewe huna wazazi?" amesema Leticia.

Aidha Mwenyekiti huyo ametoa rai kwa jamii nzima, kuacha kutumia neno waathirika pindi wanapowaita watu wenye Virusi vya Ukimwi.

"Sisi watu tunaoishi na Virusi vya Ukimwi, tumekuwa tukikwaza na neno kuitwa waathirika, neno waathirika lina unyanyapaa ndani yake, ambao ni tishio kuliko Virusi vya Ukimwi vyenyewe, tungependa tuitwe watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, kwasababu hakuna aliyetuma maombi ya kuomba ugonjwa huu", amesema Leticia.