Alhamisi , 14th Feb , 2019

Suala la ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali wadogowadogo limeendelea kuzua sintofahamu na changamoto nyingi katika mikoa mbalimbali nchini kutokana na maelezo tofauti tofauti yanayotolewa.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (kushoto) akikabidhi vitambulisho vya wajasiriamali wadogowadogo

Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kugawa vitambulisho vya awamu ya kwanza, Desemba 10, 2018 kwa wakuu wa mikoa, ugawaji wake ulionekana kwenda kwa kusuasua na hilo lilithibitishwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Januari 28, 2019 alipokuwa akigawa vitambulisho hivyo kwa awamu ya pili kwa wakuu wa mikoa.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, wakati akigawa vitambulisho vya wajasiriamali awamu ya kwanza alisema kuwa vitagawiwa kwa wajasiriamali wadogowadogo ambao mitaji yao haiziadi sh. Milioni 4.

"Mfanyabiashara mdogo mwenye mtaji chini ya Shilingi milioni 4 akiwa na kitambulisho hiki sitaki TRA, Halmashauri wala Mgambo kuwasumbua. Nawapa tu onyo msije mkachukua bidhaa za wafanyabiashara wakubwa mkawa mnawauzia ili wakwepe kodi".

"Kitambulisho kimoja ni Sh. 20,000/= hivyo kwa vitambulisho 25,000 itakuwa jumla ya Sh. 500,000,000/= na ipelekwe TRA ili wasije sema ni mradi wangu wakati mimi ni facilitator tu. Waambieni wasaidizi wenu wasiviuze kwa bei zaidi ya hii iliyopangwa", alisema Rais Magufuli.

Wakati huohuo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji hivi karibuni amewataka wajasiriamali wadogowadogo ambao mauzo yao hayavuki sh. Millioni 4 kwa mwaka kuchamgamkia fursa hiyo ili wasibughudhiwe.

Mtazamo wa kauli ya Naibu Waziri inaonesha kutofautiana na maagizo ya Rais Magufuli ambayo aliyatoa wakati akigawa vitambulisho vya awamu ya kwanza, na hicho ndicho ambacho wajasiriamali wengi wadogowadogo wamekuwa wakikilalamikia.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mkoani Tabora wamemlalamikia Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri kuwa kutokana na wafanyabiashara kutokuwa na mahesabu ya kiasi gani wanaingiza kwa mwaka na biashara nyingi kuwa za msimu na zenye faida ndogo, wanashindwa kumudu gharama ya sh. 20,000 kwa kila kitambulisho.