Jumatatu , 10th Oct , 2016

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kuwashawishi wazalishaji wakubwa wa mbolea za viwandani duniani kuja nchini kwa ajili ya kujenga viwanda vyao.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt Charles Tizeba

Wizara hiyo hadi sasa tayari imeshasaini makubaliano ya ujenzi wa viwanda vitatu vitakavyotumia malighafi ya gesi asili inayopatikana mikoa ya Kusini.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba, amesema hayo leo wakati wa mkutano wa pamoja kati ya serikali na wamiliki na wawakilishi wa viwanda hivyo unaolenga kuongeza upatikanaji wa mbolea nchini na kwamba viwanda hivyo vitajengwa katika mikoa ya Mtwara, Lindi pamoja na Pwani.

Aidha, Waziri Tizeba amesema bei ya mbolea nchini bado ipo juu ingawa wizara yake imefanikiwa kuwashawishi wazalishaji wa mbolea kushusha bei ya pembejeo hiyo na hivyo amewataka wakulima watarajie bei ya mbolea kushuka kuanzia msimu huu wa kilimo.