Jumapili , 9th Dec , 2018

Vyama vya upinzani 15 nchini vimeungana kupinga muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni mwezi uliopita wakati wa mkutano wa 13 wa Bunge.

Baadhi ya viongozi wa vyama vilivyoshiriki kutoa tamko la pamoja

Vyama vilivyoshiriki katika kutoa tamko la pamoja kupinga muswada huo ni CHADEMA, CUF, DP, ACT Wazalendo, NLD, ADC, CCK, UPDP, Chauma, NCCR Mageuzi vikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chauma), Hashim Rungwe.

Akisoma tamko la pamoja katika mkutano huo, Mwenyekiti wa muungano huo, Hashim Rungwe amesema kuwa wameamua kuichagua siku ya leo ya Uhuru kwakuwa ni siku muhimu ya kukumbukwa kwa nchi japokuwa haijasheherekewa kama ilivyozoeleka.

"Tumeitumia siku ya leo ya Uhuru kutoa tamko hili kwani ni siku muhimu kwa taifa letu na serikali ya awamu ya tano kuendelea kufuta sherehe za Uhuru ambazo Duniani kote ni siku ambayo taifa husheherekea kuzaliwa kwake, " amesema.

Kuhusu msimamo wa umoja huo kwenye sheria hiyo wanayoipinga, Hashim Rungwe ameesema hawatokubali kurudi nyuma katika kupigania haki yao hasa katika suala hili kwani wameona dalili za wazi za kutaka kupokonywa demokrasia yao waliyokuwa nayo.

Tumeona nchi nyingi zimeingia katika vurugu kutokana na wao kudai haki zao kwa nguvu ila sisi hatutaki kufanya hivyo ndiyo maana tumeamua kuudai Uhuru huu kabla hatujapokwa na kuliingiza taifa katika matatizo".

"Tunatoa wito kwa watanzania wote bila kujali rangi, kabila na itikadi zao watuunge mkono katika kuzuia sheria hii kandamizi ili kuzuia vurugu kubwa zinazoweza kutokea siku za usoni," ameongeza.

Pia Rungwe ametaja sababu za kuipinga muswada huo kuwa ni pamoja na kutokuwepo kwa uhuru wa kujiamulia na kutoshirikishwa kikamilifu katika mchakato wa kuandaa muswada huo.