Jumapili , 26th Mar , 2023

Maandamano ya kwanza katika kipindi cha miaka miwili yamefanyika Hong Kong chini ya uangalizi wa karibu na polisi.

Maandamano hayo madogo yalikuwa ya kwanza tangu China ilipoweka vikwazo vikubwa dhidi ya haki na uhuru wa watu wanaoishi katika eneo hilo.

Ni watu 100 tu walioruhusiwa kuhudhuria. Pia walitakiwa kuvaa vitambulisho vya namba na mabango yao yalichunguzwa mapema.

Maandamano ya Jumapili yalikuwa ya kupinga mpango wa kurejesha ardhi mashariki mwa mji huo.

Polisi waliwataka waandaaji kufuata masharti magumu na kuwazingira waandamanaji hao kwa kamba iliyowatenganisha na vyombo vya habari wakati maandamano yakiendelea.

Washiriki waliruhusiwa kuimba nyimbo za kupinga mradi huo. Mhudhuriaji asiyejulikana aliliambia shirika la habari la AFP kwamba mipango hiyo ilikuwa "ya kipuuzi": "Niko hapa kujiunga na maandamano, sio gwaride la aibu," alisema.