Alhamisi , 12th Jul , 2018

Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara 'Bwege' (CUF) ameweka wazi kwamba endapo kesi walizofungua yeye pamoja na viongozi wengine (Upande wa Maalim Seif) hazitamalizika mapema mpaka kipindi cha uchaguzi mkuu itabidi wafanye maamuzi magumu yeye na wabunge wenzake wa CUF kwa kuhama chama.

bendera ya chama cha Wananchi (CUF)

Mh. Bungara ameyasema hayo wakati akijibu swali aliloulizwa na www.eatv.tv ni maamuzi yapi atachukua endapo chama chao kitaendelea kuwa na migogoro na wakati huo Msajili wa Vyama anamtambua Prof. Lipumba kama Mwenyekiti na huku yeye na baadhi ya viongozi hawamtambui.

"Endapo mpaka tutafika 2020 kesi hazijatolewa maamuzi au Lipumba akashinda kesi, sisi wengine itabidi tuwe na 'plan B'. Tutaangalia mlango wa kuingia yawezekana ikawa CHADEMA, NCCR au hata NLD kwa sababu ni wenzetu ndani ya UKAWA lakini siyo kukubali kumuunga Lipumba na genge lake mkono. Kwenye maisha lazima uwe unafikiria hili na lile, hivyo hata sisi tunafikiria, ni kama gwaride filimbi ikipulizwa unageuka", amesema  Bungara.

Akizungumzia kuhusu Mamlaka aliyonayo Prof. Lipumba pamoja na Magdalena Sakaya (Viongozi wanaojulikana na Ofisi ya Msajili wa Vyama) kuwa na nguvu ya kuwavua uanachama viongozi waasiowaunga mkono, Bwege amesema wale siyo wenzao tena ndiyo maana wameamua kukiharibu chama kwa maelezo ya CCM.

"Wale wameamua kuiharibu CUF. Nipo tayari wanivue Ubunge na Uanachama lakini sipo tayari kumuunga mkono Prof. Lipumba na wala siogopi kwa lolote. Uzuri hata wapiga kura wetu hili wanalitambua kwa hiyo sina hofu kabisa" Bungara.

Mgogoro ndani ya CUF ulianza kuonekana 2015 pale Prof. Lipumba alipojiuzulu nafasi yake ya Uenyekiti wa Taifa kipindi cha uchaguzi mkuu na mwaka2016 aliporudi ndani ya chama kutaka kuichukua nafasi yake hiyo alizuiliwa kwa
mujibu wa katiba ya chama chao.