Jumatatu , 12th Sep , 2022

Wadau wa mapambano dhidi ya ukatili wa watoto na unyanyasaji wa vijana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu wameombwa kujumuika pamoja katika mapambano dhidi ya vitu vinavyohatarisha ustawi wa vijana na watoto.

Bi. Sumayi Adam, mdau wa vijana na watoto.

Rai hiyo imetolewa na wadau wa mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto na uwezeshaji vijana walipokutana na kuweka wazi mpango wa kuwasaidia vijana wakiwemo walioathirika kisaikolojia kutokana na kupitia maisha magumu katika maisha yao.

“Tupo hapa kuonesha nia yetu ya kuwasaidia vijana na watoto, kwanini ni kwasababu wanapitia madhira mbalimbali ambayo ni changamoto kwa jamii. Sawa wapo wanaotelekezwa au wanashindwa kubadilika ingawa wana ndugu zao. Wanaweza wakawepo lakini wasiwe tayari kuwasaidia. Sisi kwa kushirikiana na “Tanzanite Support Organization” tunawaalika wadau wote wanaotamani kuona vijana hawa wakibadili maisha yao, waje tuongeze nguvu ili tuijenge jamii bora"- amesema Bi. Sumayi Adam, mdau wa vijana na watoto.

Kwa upande wake Bi. Bahati Chando ambaye ni mdau wa masuala ya haki za watoto na vijana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzanite Support Organization anasema kuwa ni vema wadau mbalimbali wakajitokeza ili kuwa na nguvu kubwa katika kukamilisha mpango wa kuwasaidia vijana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.