Jumanne , 14th Mar , 2023

Wafanyabiashara watatu jijini Mwanza wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za wizi wa mamilioni ya fedha baada ya kudaiwa kuuza magari na kuhamishia fedha za mauzo hayo katika akaunti binafsi pamoja na kughushi nyaraka za uwongo za kuhamisha umiliki wa maeneo matatu tofauti jijini Mwanza

Akiwasomea mashataka 18 yanayowakabili ya wizi na kughushi nyaraka Mwendesha mashataka wa serikali Lupyana Mahenge amewataja washtakiwa hao kuwa ni Ephraem Mbogoma, Lee Burton Kweka pamoja na Happyness Robert ambae ni wakili wa kujitegemea

Inaelezwa kuwa kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2015 hadi 2021 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam mshtakiwa namba moja Ephraim Mbogoma anadaiwa kuiba dola  milioni 240 alizotumiwa kwa ajili ya kununulia magari huku katika jiji la Mwanza akidaiwa kuiba zaidi ya milioni 900 baada ya kuuza magari na kuzihamishia fedha hizo kwenye akaunti binafsi badala ya kuweka kwenye akaunti ya kampuni yao ya Litrus Tanzania Limited

Akiendelea kusoma maelezo ya kesi hiyo namba 11 ya mwaka 2023 mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza Chiganga Tengwa, Mwendesha mashtaka huyo wa serikali Lupyana Mahenge amesema mshtakiwa namba mbili Lee Burton Kweka anadaiwa mnamo mwaka 2021 kwa nyakati tofauti aliiba zaidi ya milioni 900 baada ya kuuza magari na kuhamishia fedha kwenye akaunti binafsi

Aidha mshtakiwa namba tatu Happyness Robert pamoja na washtakiwa hao namba moja na mbili mwaka 2021 wanadaiwa kughushi nyaraka za kuhamisha umiliki wa maeneo tofauti matatu yaliyopo jijini Mwanza na kuyauza na washtakiwa hao wote watatu wamekana mashtaka yote kumi na nane yanayowakabili

Baada ya kukana mashtaka hayo washtakiwa hao wakaambiwa dhamana ya mashtaka yanayowakabili iko wazi hivyo endapo watakidhi vigezo  ambapo mshtakiwa namba moja Ephraem Mbogoma alitakiwa kulipa milioni 345 au mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hiyo pamoja na kuwa na wadhamini wawili 

Mshtakiwa namba mbili Lee Burton Kweka alitakiwa kulipa shilingi milioni 225 au mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hiyo pamoja na kuwa na wadhamini wawili na mshtakiwa namba tatu Happyness Robert akitakiwa kulipa milioni kumi au mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hiyo pamoja na wadhamini wawili

Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena tarehe 27 ya mwezi huu