Jumamosi , 12th Sep , 2015

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kanda ya kati imewataka wauzaji wa vipodozi, vifaa tiba na chakula kuziondoa bidhaa zilizokwisha muda wake na kuziteketeza kabla ya kuleta madhara kwa watumiaji.

Kaimu meneja TFDA kanda kati, Florent Kyombo (kushoto) na Dk. Engelbert Bilashoboka wakisimamia kazi ya kuteketeza bidhaa

Wito huo umetolewa leo na Meneja wa TFDA kanda ya kati Florent Kyombo wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wakiteketeza bidhaa ambazo hazitakiwi kwa matumizi ya binadamu.

Amesema ni jukumu la wauzaji wa vifaa tiba, vipodozi na chakula kuhakikisha kuwa wanauza bidhaa ambazo hazijaisha muda wake na ambazo zimesajiliwa kwa matumizi ya watanzania ili zisilete madhara kwa watumiaji.

Kwa upande wake Ofisa Afya wa Manispaa ya Dodoma, Alek Balankena amewataka wakazi wa Manispaa ya Dodoma kuzilinda afya zao kwa kukataa kutumia bidhaa zilizokwisha muda wake kwa kuwa afya ni bidhaa muhimu na ambayo ikichezewa haiwezi kurudi tena.