Jumatano , 1st Mei , 2019

Ikiwa leo ni maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani, wafanyakazi nchini Tanzania wameendelea kupata pigo la kutoongezewa mishahara kwa mwaka wa nne mfululuizo, tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani mwaka 2015.

Katika maadhimisho hayo ambayo yamefanyika kitaifa Mkoani Mbeya na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, yamemalizika huku Rais Magufuli akisema kuwa hatoongeza mshahara mwaka huu, kwani ahadi yake ya kupandisha mishahara katika uongozi wake haijaisha kwa sababu bado hajamaliza muda wake madarakani.

"Ni kweli kwenye sherehe kama hizi mwaka jana niliahidi kuwa nitaongeza mishahara ya wafanyakazi kabla sijaondoka madarakani, ndugu zangu tuvumilie tu sikutaka kuwadanganya hapa kuwa nimewaongezea mishahara halafu fedha mtakazozipata hazipo, nyinyi endeleeni kuvumilia tupo katika muelekeo mzuri wa suala hili", amesema Rais Magufuli.

Ikumbukwe kwamba huu ni mwaka wa nne tangu serikali ilipotangaza kuongeza mishahara kwa mara ya mwisho, jambo ambalo limeibua malalamiko ya baadhi ya wafanyakazi, huku wengine wakiwa na mabango ya kudai kuongezewa mishahara ili waweze kumudu gharama za maisha.