Jumamosi , 26th Nov , 2022

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamadi Hassan Chande, amewataka wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini hususani Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kufanya kazi kwa ubunifu, uaminifu na uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa, ufisadi, wizi na matumizi ya madawa ya kulevya

Rai hiyo imetolewa, jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 48 ya Chuo Cha Usimamizi wa Fedha katika Kampasi Kuu ya Dar es Salaam, ambapo zaidi ya wahitimu 4,000 wametunukiwa tuzo mbalimbali

Alisema kuwa IFM imekuwa mstari wa mbele katika kuongeza idadi ya watanzania wenye taaluma na utaalamu katika Sekta ya Fedha, Uhasibu, Bima na Hifadhi za Jamii hivyo ni vema idadi hiyo iendane na kukidhi mahitaji ya soko ambayo yanahitaji wanataaluma wenye weledi na uadilifu

Mhe. Chande ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuzalisha wataalamu katika fani mbalimbali na kuliwezesha Taifa kufikia malengo yake ya kujitosheleza katika fani za fedha kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa na kijamii

Kwa upande wa Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Chande, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuongeza kiwango cha wanafunzi wanaopata mikopo mwaka hadi mwaka ili wanafunzi wenye sifa waweze kunufaika.