Waitara ahoji Makonda kutomshirikisha kwenye ziara

Jumatatu , 7th Oct , 2019

Naibu Waziri wa TAMISEMI na Mbunge wa Ukonga Mwita Waitara, amewataka wananchi wa jimboni mwake wasikubali kutumika kama daraja ili kuwasaidia wengine kupata nafasi za uongozi hii ni baada ya wananchi wa jimboni mwake,kutoa malalamiko dhidi yake kwa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ikiwemo suala la barabara.

Akizungumza leo Oktoba 7, 2019 na EATV&EA Radio Digital, Waitara amedai kuwa kabla ya kufanya ziara, Mkuu huyo wa Mkoa alipaswa kumpa taarifa kwasababu watu waliotoa malalamiko dhidi yake walisema maneno ya uongo na kwamba changamoto ya barabara hiyo ni ya muda mrefu na inajulikana.

''Mimi nilitarajia RC angeenda na watu wake, lakini wananchi wanaongea maneno yametengenezwa na ya uongo, angenipigia simu mimi kuniuliza, wamesambaza uongo yeye alikuwepo amekaa kimya, mimi napata tu kwenye mitandao na mimi siwezi kumpigia kumuuliza, lakini uzuri ni kwamba waliokuwa wanatoa tuhuma zile ukimkamata kwamba amekukashfu mbele ya jamii ivi utakuwa umeomuonea, kwasababu hakuna mtu ambaye alishawahi kuja Dodoma kunifuata mimi'' amesema Waitara.

Waitara akizungumzia suala la kuwanunulia bia wananchi wake,kila wakimuuliza kuhusu masuala ya miradi, amesema yeye siyo mjinga hadi afikie hatua kupuuzia kusikiliza kero za wananchi wake.

''Kwa akili ya kawaida ni kiongozi gani utaambiwa habari ya changamoto ya eneo lako uzungumze habara ya bia na huyo mtu sijawahi kumuona popote pale,hakuna mtu wa Kivule anaweza kusema vile, huenda hanijui vizuri atakuwa amesimuliwa, mtu ambaye ananifahamu hawezi kusema hivo na mimi muda wote niko jimboni kwangu alikuja Dodoma kufanya nini?'' amesema Waitara.

Hatua hii imekuja ikiwa ni masaa machache yamepita tangu wananchi wa Jimbo la Ukonga kutoa malalamiko dhidi yake kwamba, mara nyingi hasikilizi kero za wananchi wake na ikitokea wamemuuliza huwazuia na kuwanunulia bia.