Jumatano , 31st Dec , 2014

Matukio ya kutishia amani ya nchi na usalama wa raia yatapungua kama mabalozi wa nyumba kumi watafanya kazi zao kwa uaminifu kwani wao ni viongozi wa kwanza walio karibu na wananchi hivyo basi wanatakiwa kuwafahamu wakazi wa maeneo yao.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema Balozi ni kiongozi wa kwanza anayetakiwa kujua idadi ya wakazi wake, kazi wanazozifanya na majina yao kitendo ambacho kitasaidia kuimarisha usalama wa eneo husika lakini miaka ya hivi karibuni wameacha kufanya kazi hiyo kwa uadilifu na kuviachia vyombo vya dola pekee.

Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete alisema mabalozi ni msingi na nguzo ya chama bila ya mabalozi chama hakiwezi kwenda vizuri ni kama vile binadamu anaweza kuwa na kila kitu lakini kama hana miguu hawezi kutembea.

Akiongea kwa niaba ya wajumbe walioshiriki semina hiyo Rashid Thabit kutoka kata ya Rahaleo alishukuru kwa mafunzo waliyoyapata na kusema kuwa yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi.

Semina hiyo ya siku moja iliyohudhuriwa na wajumbe 993 kutoka kata zote 18 za wilaya hiyo iliandaliwa na Mama Kikwete ambaye aliwaahidi mabalozi kuwapa mafunzo hayo ili wajue majukumu yao ya kazi.

Mada zilizojadiliwa ni kazi na wajibu wa mabalozi na katiba mpya iliyopendekezwa.