Alhamisi , 19th Mei , 2016

Mbunge wa Mtwara Mjini Maftaha Nachuma CUF ameeleza Bungeni Mjini Dodoma katika Mkutano wa Bunge unaoendelea kwamba watendaji wenye mamlaka ya kusoma mita za maji mkoani humo hukadiria na kuwabambikizia wananchi madeni.

Mheshimiwa Spika Wizara inafahamu jambo hili ambapo wakati waziri anakuja mkoani Mtwara wananchi walimpokea kwa maandamano wakieleza kero ya watendaji wa idara ya maji kuwabambikia madeni kwa kutosoma mita na badala yake kukadiria matumizi ya maji kwa wananchi hao jambo ambalo linazua malalamiko mengi, ni ipi kauli ya serikali juu ya jambo hili?

Kufuatia tuhuma hizo za Mbunge huyo Waziri wa Maji Mhandisi. Gerson Lwenge amesema jambo hilo ni baya na ni kinyume na sheria kwa kuwa kila mwananchi anapaswa kulipia maji kulingana na matumizi na sii vinginevyo.

Waziri Lwenge ameongeza kuwa kitendo hicho kinapaswa kuachwa kwani huko ni kuwaumiza wananchi na hivyo maagizo ya serikali yafuatwe kuanzia sasa.