Ijumaa , 25th Dec , 2015

Wakulima wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wameipongeza serikali kwa kuwawezesha kupata mbegu mpya za kisasa za mhogo zitakazowawezesha kupata mavuno mengi zaidi na kuwa na uhakika wa chakula tofauti na mbegu walizokuwa wakitumia awali.

Mratibu wa utafiti wa zao la Muhogo kitaifa Dkt. Godfrey Mkamilo

wakizungumza wakulima wa zao la mihogo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wamesema mbegu hizo mpya aina ya gunia zilizofanyiwa utafiti wa kutosha na watafiti kutoa Naliendele mkoani Mtwara, zitawawezesha kuvuna mihogo mingi.

Wamesema hapo awali walikuwa wakipata mavuno kidogo na kushindwa kukidhi mahitaji yao na familia zao, ikizingatiwa zao hilo limekuwa likihimili ukame, huku wafanyabiashara wa mazao yatokanayo na mhogo wakipongeza hatua za watafiti kukuza uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Mratibu wa utafiti wa zao la Muhogo kitaifa Dkt. Godfrey Mkamilo amesema mbegu hiyo iliyotafitiwa ina ubora na uwezo wa kuzalisha zaidi tofauti na mbegu zingine na kwamba wanakusudia mbegu hiyo ienee katika maeneo mengi hapa nchini ili kusaidia wananchi kujikwamua na umasikini na uhaba wa chakula na kwa sasa wanaendelea na utafiti kwa kushirikisha nchi nyingine kupata mbegu bora zaidi zinazohimili magonjwa.