Ijumaa , 8th Jul , 2016

Wanafunzi wenye ulemavu katika shule ya msingi Patandi iliyopo wilaya ya Arumeru, Arusha wamelalamikia tatizo la upungufu wa walimu,vitabu na vifaa vya kufundishia kwa wanafunzi hao wenye mahitaji maalumu hali inayokwamisha maendeleo ya kitaaluma.

Mwanafunzi asiyeona anayesoma darasa la saba Clara Damian

Mmoja wa wanafunzi asiyeona anayesoma darasa la saba Clara Damian, amesema kuwa kumekuwa na uhaba wa vitabu kwa watoto wasioona na mashine za kuandikia maandishi yenye nundu ambazo ni chache na kwa sasa ni mashine tatu pekee zinafanyakazi ikilinganisha na idadi kubwa ya wanafunzi.

Ameeleza kuwa miundombinu ya majengo ya madarasa pia yamekuwa si rafiki kwa watoto wenye ulemavu hivyo anashauri miundombinu ya majengo na shule iendane na mahitaji wa watoto hao.

Mratibu wa Kitengo Cha Walemavu Mwalimu Anna Shayo katika shule hiyo amekiri kuwepo kwa upungufu wa walimu na vitabu kwa watoto wenye mahitaji maalumu na kuiomba jamii,taasisi na serikali kushiriki katika kuboresha maendeleo ya watoto hao ambao wakijengewa misingi bora ya elimu wanaweza kuwa na mchango kwa jamii.