Alhamisi , 24th Mar , 2016

Watu 3 ambao ni walinzi wa Suma JKT wanashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kufuatia kuhusishwa na wizi wa kompyuta zinazokadiriwa kuwa 50 mali ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) huku mmoja wa askari polisi akihusishwa katika tukio hilo.

Jengo la Utawala Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM).

Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa wizi huo ulitokea juzi baada ya wanafunzi wa chuo hicho kufunga chuo kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu ya pasaka.

Amesema kuwa katika wizi huo baadhi ya walinzi wa Suma JKT ambao ndiyo wanajukumu la kulinda chuo hicho walihusika ambapo baadhi yao wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Imeelezwa kuwa katika tukio hilo kuna baadhi ya askari kutoka katika kituo cha kati cha polisi mjini hapa walihusika katika wizi huo hali ambayo inaleta mkanganyiko katika uchunguzi wa tukio hilo.

Akizungumzia tukio hilo Ofisa habari wa Udom, Beatrice Baltazar amesema ni kweli kuna wizi wa kompyuta umetokea kwenye chuo hicho lakini bado hajajua idadi kamili ya kompyuta zilizoibiwa na kubainisha kuwa walinzi watatu wa Suma JKT wanashikiliwa kutokana na wizi huo.

“Ni kweli kuna wizi wa kompyuta hapa chuoni lakini bado sijajua idadi kamili ya kompyuta zilizoibiwa ila kuna walinzi watatu wa Suma JKT wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano kwa kuwa kati yao kuna wanaohusika katika wizi huo,” alisema Beatrice.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alipoulizwa kuhusiana na suala hilo kwa njia ya simu alisema kuwa taarifa hizo anazo lakini hana maelezo zaidi kwa kuwa yuko likizo na kusema kuwa hakuna askari polisi aliyehusika katika tukio hilo bali ni walinzi wa Suma JKT.

“Hapana hakuna askari wetu aliyehusika katika tukio hilo… wenye jukumu la kulinda chuo hicho ni walinzi wa Suma JKT na hao ndiyo wanaoshikiliwa kwa mahojiano zaidi…. hakuna askari wetu aliyehusika,” alisema Mambosasa.