Jumanne , 11th Aug , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema ukosefu wa vyoo katika Shule ya Msingi Sisimba ni aibu kwa waliosoma katika shule hiyo na hivyo ametoa wito kwa wananchi kuanza kuchangia ujenzi wa vyoo kabla yeye hajaanza kuwasaka wale waliosoma mahali hapo ili wachangie kwa lazima.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila.

RC Chalamila ameongeza kuwa shule kubwa kama hiyo haina choo cha watoto wa kiume ,lazima itafutwe namna kwa watu waliosoma shule hiyo kuleta fedha kwa lazima.

"Tumekuja tuoneshane aibu tuliyoitengeneza, aibu ambayo shule kubwa kama Sisimba waliyosoma watu mbalimbali leo haina hata choo cha watoto wetu wa kike wala choo cha watoto wa kiume, lakini huko mtaani watu wanasema Serikali yao hiyo, lakini lazima tutafute namna ya wao kuchangia shule hii kwa lazima", amesema RC Chalamila.

Aidha RC Chalamila ameongeza kuwa, "Unajua muda wa kubembelezana sana katika Taifa hili umepitwa na wakati unafanya biashara Mbeya ndiyo umesoma Sisimba peleka Milioni 1, hiyo fujo nitaifanya muda si mrefu, hutaki kukaa Mbeya bora uondoke kwa sababu hapa napo tunajitosheleza".