Wanachuo walia, tunapiga deshi, hatupewi chakula

Alhamisi , 13th Feb , 2020

Wanachuo wa Chuo cha Afya Kagemu ambacho kinamilikiwa na Serikali wamesema wanakabiliwa na changamoto ya kushinda na kulala njaa wawapo chuoni, kutokana na chuo hicho kutokuwa na mfumo rasmi wa kuwapatia chakula.

Wanafunzi wa Chuo cha Afya Kagemu, wakizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt Zainabu Chaula.

Wakitoa malalamiko yao mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Zainabu Chaula aliyefanya ziara chuoni hapo, wanachuo hao wamesema kuwa hali hiyo inasababisha baadhi yao kushindwa kukamilisha masomo yao, huku wengine wakidai ufaulu wao kushuka.

Sebastian John ni miongoni mwa wanafunzi katika chuo hicho ambapo wamesema "Mpaka inafikia mwanafunzi anashindwa kula chakula siku nzima au siku nyingine anapata mlo mmoja, mara nyingi tunatumia lugha yetu nzuri ya kuwa tunapiga deshi".

Kutokana na changamoto hiyo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainabu Chaula amesema kuwa Serikali imepokea malalamiko ya wanachuo hao na kuwa ili kuwapunguzia adha hiyo itaanza na ukarabati wa bwalo la chakula na jiko ili kuwawezesha kupata chakula chuoni.