Jumanne , 19th Jul , 2016

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameeleza kuwa fedha kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo zitatolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa wanafunzi waliombewa fedha hizo toka vyuo mbalimbali hapa nchini.

Prof. Ndalichako ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya ucheleweshwaji wa fedha hizo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Prof. Ndalichako amesema kuwa kuna zaidi ya wanafunzi 2,736 hewa ambao majina yao yamewasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya kulipwa fedha za mafunzo kwa vitendo, yakiwemo majina ya wanafunzi waliofariki na waliofukuzwa chuo.

Aliendelea kwa kusema kuwa, kuna chuo ambacho kilituma ripoti ya wanafunzi waliofukuzwa chuo mwaka 2013/2014 lakini majina hayo yametumwa tena kwa ajili ya kupewa fedha za mafunzo kwa vitendo kwa mwaka huu.

Ameongeza kuwa kutokana na kasoro zilizojitokeza katika majina ya wanafunzi wanaotakiwa kupewa fedha kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo Prof. Ndalichako amesema kuwa serikali haitatoa fedha mpaka uhakiki wa wanafunzi wanaotakiwa kupata fedha hizo utakapo kamilika kwa vyuo vyote nchini.

Aidha, Mhe. Ndalichako amesema kuwa majina ya wanafunzi hao hewa yamewekwa katika mitandao wakitakiwa kujihakiki TCU ili kujiridhisha kama kweli ni wanafunzi na wanaendelea na masomo.

Hata hivyo , Prof. Ndalichako amevitaka vyuo vikuu kutoa ushirikiano kwa timu zilizotumwa katika vyuo vyao kufanya uhakiki wa wanafunzi wanaotakiwa kupata fedha hizo kwani kuna baadhi ya vyuo vimekuwa havitoi ushirikiano kwa kisingizio cha kuwepo kwenye mitihani.