Wanafunzi wa darasa la 7 waliofutiwa matokeo

Jumanne , 15th Oct , 2019

Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), limeyafuta matokeo ya watahiniwa 909, waliobainika kufanya udanganyifu katika Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi na kuagiza mamlaka kuwachukulia hatua, wale wote waliohusika kufanya udanganyifu katika mitihani hiyo.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt Charles Msonde

Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 15, 2019 na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt Charles Msonde, wakati akitangaza matokeo ya Darasa la Saba kwa mwaka 2019, ambapo ufaulu umepanda kwa asilimia 3.78, ukilinganisha na mwaka 2018.

Aidha tathmini ya awali ya matokeo hayo imeonesha kuwa ufaulu katika somo la Kiingereza bado uko chini, ukilinganishwa na masomo mengine licha ya kuwa unaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka na kwamba juhudi za makusudi zinahitajika ili kuinua kiwango cha ufaulu wa somo hilo.

Jumla ya watahiniwa 947,077 wa Shule za Msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 495,937, sawa na asilimia 52.37 na wavulana 451,140 sawa na asilimia 47.63, huku watahiniwa wenye mahitaji maalumu  wakiwa 2678 sawa na asilimia 0.23.