"Wanahangaika tu kutuchonganisha"- Makonda

Jumatano , 14th Feb , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amefunguka na kumuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutosikiliza maneno ya mashetani ambao wanataka kuwachonganisha baina yao ili wasiweze kupatana katika utendaji kazi wao.

Makonda amezungumza hayo wakati akitoa salamu kwa wananchi waliohudhuria uzinduzi wa jengo la huduma za mama na watoto kwenye hospitali ya Amana Jijini Dar es Salaam, lilogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.2  ambapo mgeni rasmi alikuwa Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

"Nikuombe Mhe. Waziri Mkuu kuna gazeti moja linahangaika sana kuandika habari mbaya mbaya za mkoa wa Dar es Salaam, lisikupotezee muda hata kulisoma. Wanahangaika tu kutuchonganisha huku na kule, Mungu awahurumie tu kwa sababu hawajui walitendalo", amesema Makonda.

Pamoja na hayo, Makonda ameendelea kwa kusema "lakini niwakumbushe tu kwamba aliyeanza kuchonganisha duniani anaitwa shetani, kuna watu raha zao wasikie labda Mahakama imesema kauli ya kunikashifu au kunitukana Mkuu wa Mkoa. Waelewe tu hawatofanikiwa".

Kwa upande mwingine, Makonda amemsisitizia Waziri Mkuu kutowasikiliza watu wa aina hiyo na kumuomba wachape kazi.