Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde
Wito huo ameutoa mkoani Iringa aliposhiriki uzinduzi wa mradi wa kuwawezesha vijana na wanawake katika mnyororo wa thamani wa kilimo awamu ya pili (Generation Food Accelerator II) chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa Agri-connect.
"Ni dhahiri kwamba ninyi wadau, mkishirikiana na serikali katika kutekeleza miradi yenu, kutaleta tija kubwa zaidi kutokana na kwamba, kutazuia upelekaji wa rasilimaji fedha katika eneo hilo hilo moja kwa serikali na wadau wa sekta binafsi," amesema Naibu Waziri Mavunde
Aidha Naibu Waziri Mavunde ameongeza kuwa, "Changamoto zinazowakabili vijana katika kilimo zinafahamika zikiwemo ukosefu wa ardhi, mitaji, pembejeo, miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi na masoko ya uhakika ya mazao watakayozalisha,"
Awali, akitoa wasilisho, Mratibu wa mradi huo Ronald Mtana alieleza kuwa mradi huo ambao utawafikia vijana 30,000 wenye thamani ya shilingi milioni 726 utatekelezwa kwa awamu katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Katavi.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uzalishaji Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Beatrice Banzi alieleza umuhimu wa sekta binafsi kuchangia jitihada za serikali kutatua changamoto za vijana na kutoa wito kwa wadau wote wenye utayari kujiunga katika utekelezaji wa programu ya kuwezesha vijana kushiriki kilimo chenye tija.

