Jumatatu , 13th Sep , 2021

Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka wanaume kuunda vikundi vya kujadili changamoto wanazokumbana nazo na kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kuijenga jamii yenye usawa na yenye kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake.

Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima, alipomtembelea Mama Zaina Khamis, aliyetelekezwa na mme wake

Wito huo ameutoa alipomtembelea Mama Zaina Khamis mwenye watoto 6 waliokosa fursa ya kupata elimu licha ya kuwa umri wao unastahili kuendelea na masomo anayeishi na wanaye katika Kata ya Bangulo Gongo la mboto, baada ya kutelekezwa na mume wake aliyekuwa akiishi nae Tabata. 

"Wajibu wa vyombo vya serikali lazima tujisogeze karibu na wananchi, wananchi watujue ili wajenge imani na sisi kwamba tupo karibu nao, sasa hivi tuna simu za mkononi, tuna mitandao ya kijamii tuitumie vizuri ," amesema Dkt. Gwajima. 

Kufuatia hatua hiyo Dkt. Gwajima akasema kwamba, Mama Zaina atachukuliwa na kuhifadhiwa na serikali kwenye makao maalum na salama katika kipindi hiki ambacho watoto wake wakiendelea kufanyiwa utaratibu wa kujiunga na masomo, huku wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wakiendelea kutafuta suluhu ya changamoto ya mzazi mwenza ili kuinusuru familia hiyo.